Wanafunzi na walimu wa Hawzah ya Hazrat Zaynab (a.s.) iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, wamefanya Majlisi ya maombolezo ya Tasu'a ya Imam Hussein (a.s.), iliyojumuisha hotuba, usomaji wa majonzi, Ziara ya Ashura, Ziara ya Waritha na Surah Yasin kwa lengo la kuhuisha kumbukumbu za Karbala na dhulma iliyowapata Ahlul-Bayt (a.s).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA–, Hawzah ya Hazrat Zaynab (a.s.) iliyopo Kigamboni, Jijini Dar es Salaam, imefanya Majlisi ya maombolezo ya Tasu'a ya Imam Hussein (a.s) siku ya Alhamisi, tarehe 25 Juni 2026, inayosadifiana na tarehe 9 Muharram 1448 Hijria.
Majlisi hiyo iliandaliwa kwa lengo la kuhuisha kumbukumbu za Tasu'a na kukumbuka matukio ya kusikitisha yaliyowakumba familia ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) katika ardhi ya Karbala.
Programu hiyo ilianza kwa kusomwa kwa aya kadhaa za Qur'ani Tukufu na mwanafunzi Jamilah Omar, ikifuatiwa na hotuba ya kwanza iliyotolewa na mwanafunzi Muanidi Sultan, huku hotuba ya pili ikitolewa na mwanafunzi Amina Haruna.
Aidha, mwanafunzi Sakina Shaaban alisoma majonzi na masaibu ya Karbala, akiwakumbusha washiriki matukio yaliyopelekea kuuawa kwa Imam Hussein (a.s.) na wafuasi wake katika jangwa la Karbala.
Washiriki wa majlisi hiyo pia walisoma Ziara ya Ashura, Ziarat al-Waritha na Surah Yasin, kabla ya kuhitimisha kwa maombolezo ya Tasu'a ya Imam Hussein (a.s.).
Jumla ya Wanafunzi 144, wakiwemo wanafunzi pamoja na wasimamizi wa bweni, walishiriki katika hafla hiyo ya kiroho iliyoandaliwa na Shule ya Wasichana ya Hazrat Zaynab (a.s.) ya Kigamboni, Tanzania.
Waandalizi wa majlisi hiyo walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ujumbe wa Karbala, kuimarisha mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s) na kuwafundisha vijana maadili ya kujitolea, subira na kusimama dhidi ya dhulma kama alivyofanya Sayyid wa Mashahidi, Imam Hussein (a.s).
Your Comment